|
|
|
![]() ![]() |
||
|
Gazeti la INJILI Kwenye Internet http://munishi.netfirms.com Tel. 254722602445 E-mail:fmunishi@hotmail.com Or munishifaustin@yahoo.com Tumaini Jema 28-2-2003 Hii ni Injili tumaini la uzima.Ukiiamini itakuokoa kutoka katika utumwa wa shetani.Ukiikataa ole wako, Kwani umeikataa nguvu pekee ya Mungu kukuwezesha kumshinda shetani duniani.Ukisema utangojangoja, hujui lini adui yako shetani amepanga kukushambulia na magonjwa pamoja na matatizo mengine.Injili ni bima ya maisha duniani na mbinguni. Una hakika ya kulipwa mema, ndiyo maana matumaini yetu katika Injili hayafifii.Kila siku tunatarajia mema kutoka kwa Mungu. Twatarajia japo hatujapokea, Ndiyo maana tuna TUNAINI JEMA kwamba tutapokea tunayoyatarajia. Ukombozi wa miili yetu kutoka katika mitego yote ya shetani, Na mwisho uzima wa milele ambao Mungu alituahidi tumpendao na kuitii amri yake ya kuihubiri Injili kwa kila kiumbe duniani. Tunafanya hivyo kwa ujasiri na tumaini jema, Kwani Mtume Paulo anakiri haya katika kitabu cha Warumi 1:16 Kwa maana siionei haya Injili, Kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye. Lengo kuu la Injili ni wokovu. Siyo kelele nyingi, wala siyo kujaza watu katika majumba ya ibada.Itawafaidi nini kuwa wengi kanisani wakati wokovu lengo kuu la injili mnalikataa? Je wingi wenu utawafanya mhesabiwe haki mbele za Mungu? Hapana. Tunahesabiwa haki kwa imani baada ya kutubu dhambi na kumkana shetani. Fundisho la kutubu dhambi ndilo msingi wa Injili ya Yesu. Msilikwepe, wala msilirahisishe ili kulinda umati kanisani. Ni haki yenu kuisikia Injili kama ilivyo na pia ni haki yenu kuamua kuipokea au kuitupilia mbali. Tusipoihubiri Injili kama ilivyo, tunawanyima haki yenu ya kuisikia injili. Siyo ajabu umebaki mchanga kiroho miaka yote.Kuna mtu aliyekunyima haki yako ya kuisikia Injili. Chakula cha ROHO ni Injili na siyo maneno matamu yenye lengo la kukubariki kibandia na ubaki mtumwa wa dhambi. Unaambiwa Bwana awe nawe, na wewe unajibi awe pia nawe. Mwisho huyo Bwana anabaki katikati yenu kwani wote mmekataa aingie mioyoni mwenu, awaonyeshe makosa yenu, Mtubu mpate msamaha wa dhambi . Mnapenda vitu rahisi ndiyo maana Mungu amewapa akili na hamtaki kuzitumia. Kila kitu kwenu mnatajia muujiza. Shetani amewajua. Ndiyo maana akiwatumia baathi ya wahubiri, Siku hizi injili imegeuzwa kama karata ya pata potea. Weka hapa upate au ukose. Nina maana ya TOA UBARIKIWE. Ndiyo iko katika maandiko, Lakini ilimaanisha Hivyo? Kwamba washirika wamtegemee Mungu na wachungaji wawategemee washirika? Nani aliye katika nafasi nzuri zaidi ya kumtegemea Mungu. Mchungaji? au Mshirika? Kondoo wanaambiwa wamtegemee Mungu kupata malisho, Lakini Mchungaji anawategemea kondoo kupata maziwa. Wanakamuliwa na walipo ni jangwa hakuna majani. Badala wapelekwe kwenye malisho, Wanawekwa jangwani, Na wanayoyasikia ni toeni mbarikiwe. Wanafanya kama walivyoambiwa, Na miaka inapita huku hali yao ikizidi kuwa mbaya. Wengine wanakufa kabisa kiroho na kurudi dhambini, wengine hawatoki lakini wanafanya mbinu za kutafuta malisho, Wengine wanakaa lakini hawaendelei kiroho wala kimwili. Wengi wanaamua kuwa watalii wa kiroho. Leo wako hapa, kesho wako pale. Wachungaji wala hata hawasikii chochote.Wakitoka hawa wengine wanakuja. Maziwa hawakosi. Kanisa limegeuka kama gari la abiria. Linabeba likishusha. Wakitoka wanaingia. Hapana haipaswi kuwa hivyo. Kanisa ni mwili wa Kristo. Ni mali ya Yesu na siyo mali ya mchungaji. Kanisa lilinunuliwa kwa gharama kubwa. Mwokozi Yesu alilinunua kwa Damu yake. Wachungaji tumepewa dhamana tu ya kulisha kondoo. Wanaruhusiwa kukua kiroho hata kumfikia na kumpita Yesu. Je sisi ni kina nani tusiulizwe maswali na washirika? Hasa yanayohusu pesa na matumizi yake. Mitume walikuwa na vitu vyote shirika. Mapato ya Kanisa ni mali ya jumuia husika na siyo mali ya mchungaji aitumie apendavyo. Hata kama alienda ngambo kikanisa akapewa zawadi ya pesa taslimu, gari au vyombo, Hiyo ni mali ya KANISA na siyo mali yake binafsi na jamii yake. Inashangaza kuwaona wachungaji wengi wakiwa matajiri wa kutisha wakati washirika ni masikini wa kutupwa. Kweli inatakiwa kuwa hivyo? wale wanaochunga mifugo kama ngombe na mbuzi, ni kawaida kuwarudisha mifugo zizini wakiwa na njaa na huku wao wameshiba? Hapana ni kinyume chake.Mungu atusaidie ili tuwalishe kondoo wake chakula cha kiroho watubu dhambi na waukulie wokovu. Yesu anarudi mapema kuliko tunavyofikiri.Anakuja kulichukua kanisa lake alilolinunua kwa damu yake. Wachungaji mtajibu nini siku hiyo? Tuseme Yesu aamue ghafla kuja kutembea hapa duniani kuikagua kazi yake. Aingie makanisani akute sarakasi fujo na kelele zinazoendelea huko. Unafikiri atafanyaje? Halafu atoke nje kulitembelea jiji la Nairobi. Akute kila kona ya barabara kuna vyombo vya kupaza sauti na kinachosikika huko ni "Toeni Mtabarikiwa Kesho." Akute wengine wakisema "Yesu nguvu zake hazisimamishi tena bali zinaangusha watu chini. Njoni niwaguse tu na mtaanguka mkiwa wagonjwa na wenye dhambi, na mkiamka mtakuwa hivyo hivyo." Sijui Yesu mwenyewe angewaambiaje, Lakini sina mashaka atachukua kiboko na kuwatimua kama alivyofanya kwa wale waliokuwa wakiuza na kununua kwenye nyumba ya baba yake. Hata kama MAVUNO ni mengi na watenda kazi ni wachache, Haina maana kwamba sasa tutakubali kila aliyekosa la kufanya aanze kuingia shambani kuvuna. Ndivyo ilivyofanyika na badala ya kuvuna wameharibu mazao.Mengine wameyakata vibaya, Mengine wameyatawanya, Mengine wameyaharibu wala hayafai kuvunwa tena. Siku hizi wale tunaowaita wasiyoamini siyo watu ambao hawajaisikia injili, Ni wale waliyokwisha ingia makanisani, wakasikia porojo badala ya injili, wakaambiwa toeni mbarikiwe wakatoa na hawakubarikiwa, yakawafika shingoni wakatoka. Sasa kazi ya kuwarudisha inakuwa ngumu. Wanasema walishaumwa na nyoka wakiguswa na nyasi wanashituka. Wana haki ya kufanya hivyo kama wanadamu, Nami niko hapa kuwapa tumaini jema. Walisikia vibaya wakakosa tumaini, Leo wamesikia vizuri ili wapate matumaini. Tuombe Bwana Yesu Mchungaji mwema. Iangalie kazi yako. Litupie jicho kanisa lako. Ulisema mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache. Hukusema tuingie kiholela kuifanya kazi ya kuvuna, Bali ulisema tukuombe Bwana wa mavuno uwatume watendakazi. Ndiyo maana tunakuomba leo uwatume watendakazi katika shamba lako. Wale uliotuita tayari, tupe uamsho mpya na mbinu mpya hasa ya kuweza kuyarudisha mavuno yaliyoharibiwa na wavunaji bandia.Tusaidie watumishi wako tuweze kuinena injili yako kama ilivyo. Tusiongeze wala kupunguza kitu. Tunayatumia mamlaka uliyotupa ya kufunga na kufungua. Tunamfunga Shetani anayeleta mafarakano katika Kanisa lako. " Shetani Najua unanisikia. Nakuamuru katika Jina la Yesu utoke ndani ya watumishi wa Mungu na uwaache waihubiri Injili kama ilivyo." Hatukosi kuzijua hila na mbinu zako za kuchinja na kuua. Ndiyo maana wengi umewafunga katika minyororo ya magonjwa mbali mbali. Tunaikata minyororo hiyo kwa jina la Yesu. Wawe huru sasa, tena wawe nao tele. Ikiwa wewe ni mgonjwa, Weka mkono wako unapoumwa sasa. Maombi haya yatakugusa hapo ulipo na utakuwa mzima kabisa. Kumbuka yote hayo ni bure. hitajiki kulipa chochote. Tuendelee kuomba. Baba katika jina la Yesu unawaona hawa walioonewa na adui shetani. Ni wagonjwa katika ROHO na miili yao. Waponye katika jina la Yesu. Hasa ugonjwa wa roho kutokukupokea wewe. wanapofanya uamuzi wa kuyakabithi maisha yao kwako, Wapokee. Wasamehe. Yaandike majina yao katika kitabu cha uzima. Wape uwezo wa kufanyika watoto wako wapendwa. Zaidi ya yote waponye kabisa magonjwa yao. Ninakushukuru kwa sababu ninaamini kwamba umenisikia mtumishi wako. Pia ninaamini kwamba umewasamehe wote waliokuita kwa imani na tumaini jema. Nakushukuru pia kwa kuwaponya wagonjwa wote. Umewaponya kwa sababu unawapenda. Umewaponya ili wakutumikie. Umewaponya kwa kuwa wewe ndiye Mungu wa pekee kwao na hawana mwingine wa kuwaponya. Ndiyo ili waujue ukuu wako. Tena umewaponya ili wajue kwamba duniani wala mbinguni, Hakuna Mungu kama wewe.Tunakutukuza kwa wema wako. Tunakushukuru kwa fathila zako kwetu. Tunaupokea uponyaji kwa mioyo iliyo na furaha tele. Hata kama kuna wengine wenye matatizo mengine ambayo siyo magonjwa, Wasaidie wote. Wasio na kazi wapate kazi. Waliofiwa na waume au wake au na wawapedao katika jamii zao, uwafariji. Walio na kesi za mashamba mahakamani pia wasaidiwe ili watendewe haki. Waliofutwa kazi kwa hila, wasaidie wapate kazi ili adui zao wajue kwamba yuko Mungu anayewasaidia walioonewa bure. Wenye chokochoko katika ndoa zao wape suluhisho la kudumu kwani wewe ndiye mwanzilishi wa jamii kwa ndoa takatifu.Wakuu na watawala wa dunia hii waonyeshe kwamba wewe ndiye unayetawala dunia ukiwatumia watumishi wako. Wajalie watumishi wako nguvu zitokazo kwako ili kila mamlaka ikutii wewe Mungu mkuu. Ishara na Miujiza ziambatane na watumishi wako kama ishara pekee kuonyesha ndiwe uliyetutuma. Tumeomba hayo machache katika jina kuu kupita majina yote, Jina la Yesu mwokozi wetu. Amen. |
||||||||||||
|
|
|
|