Free Web Hosting by Netfirms
Web Hosting by Netfirms | Free Domain Names by Netfirms


Ukurasa wa mbele
Gazeti la NYAKATI
Soma barua Yahoo
Soma barua Hotmail

Gazeti la INJILI
Kwenye Internet

http://munishi.netfirms.com

Tel. 254722602445 E-mail:fmunishi@hotmail.com Or
munishifaustin@yahoo.com

Tumaini Jema 21-3-2003

Wapendwa katika ushirika wa Yesu Kristo. Ni matumaini yangu kwamba hamjambo na baraka za Bwana ni tele maishani mwenu. Karibuni tuwe pamoja katika kipindi cha tumaini jema. Usijali unayoyapitia maishani, Mungu aliyaona yakija. Kwamba hakuyazuia, Inaonyesha jinsi alivyo na imani nawe kwamba utashinda katika hilo. Malaika watashangilia utakapovuka katika hilo bila kumkana Mungu. Shetani atainamisha kichwa kwa huzuni utakaposimama imara mpaka mwisho. Simama kwani tuliye naye ni mkuu kuliko aliye ulimwenguni. Kama Yesu alivyoshinda, Nasi alitupa uwezo wa kuwa zaidi ya washindi, Kwani kazi kubwa aliimaliza pale msalabani. Ni ujumbe wa matumaini kwako. Uinue roho yako, Uchangamke uushangilie wokovu wa Bwana. Karibu na pambazuko giza huwa nene zaidi, Pia karibu na mafanikio yako, vikwazo huwa vingi. Usitishwe na vikwazo, Bali kaza mwendo kuyaendea mazuri Bwana aliyokuwekea mbele yako. Usiangalie nyuma, Kwani siyo kawaida ya Mungu kuweka baraka zetu nyuma. Mbele daima, Na nyuma mwiko. Hayo ndiyo matumaini ya kutuingiza kwenye ufalme wa milele mbinguni. Ufalme usiyo na vita na machafuko kama tunayoyasikia duniani. Huko hakuna hitaji la mafuta kutufanya tupigane vita kumbe kiini ni mafuta. Tena hakuna soko la kuuza dhahabu, Kwani barabara za huko ni dhahabu. Tena hakuna maadui wa kudumu huko, Kwani wote watakaoingia huko hawatakuwa na sababu ya kuwa na maadui. Adui yetu alikuwa shetani, na katika ufalme wa Mungu haruhusiwi kuingia. Usiniulize maswali, Kwani Mungu aliyesema kwa kinywa cha Yesu tuwapende adui zetu, Ndiye aliyemwandalia Adui yake shetani ziwa la moto na haitabadilika tumuone shetani mbinguni.

Tusome Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo Mtakatifu sura ya 5:43-47 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na umchukie adui yako. Lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, Waombeeni wanaowauthi, Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; Maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, Huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, Mwapata dhawabu gani? Hata watoza ushuru je hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, Mwatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Mungu ni mkamilifu, Ndiyo maana kwake kutokumsamehe shetani siyo kitu tunachoweza kumuuliza. Ukamilifu wake unatetea maamuzi yake ya kumhukumu shetani. Udhaifu wetu kama wanadamu unatuhukumu tunapowahukumu wenzetu. Kipimo tosha kuweza kuwahukumu wenzetu, Ni ukamilifu wetu katika suala tunalojaribu kuwahukumu wengine. Ikiwa sisi wenyewe ni dhaifgu katika suala husika, Ndipo ujasiri wa kuwahukumu wengine unapokosekana. Hata kama tutajaribu kufanya hivyo kwa sababu ya uwezo wetu kipesa, Bado kelele zitasikika kutoka kila kona kwamba hatuna ukamilifu wa kutosha kuhukumu hayo. Mnaisikia dunia nzima ikipiga kelele kwamba Amerika haina ukamilifu wa kutosha kuweza kuhukumu wanayohukumu duniani. Sharti moja la kutimiza ndipo tuweze kuwahukumu wengine, Kwanza lazima tuwe wakamilifu katika yale tunayowahukumu wengine kwayo. Vinginevyo Mungu hatatuelewa, na mbaya zaidi wanadamu wenzetu hawatatuelewa. Yesu anaposema tuwapende adui zetu, Ana maana kwamba mengi yaliyosababisha uadui hata wenyewe siyo wakamilifu katika hayo.

Mungu atusaidie ili tuwe wakamilifu kama yeye alivyo. Nasema tusaidiwe ukamilifu kwani maovu ni mengi duniani. Kukikosekana wakamilifu waliohitimu kuyakemea, Maovu yatazidi na kushamiri. Haijalishi ni wanafiki wangapi wanaowahukumu wenzao kama Amerika wanavyofanya, Lakini hiyo haitamaliza maovu, kwani wanaojaribu kuyakemea na wenyewe ni waovu kuliko wanaowakemea. Msidanganyike. Waovu hawawezi kuumaliza uovu. Amerika ni waovu. Nina ujasiri wa kusema kwamba hawajahitimu kukemea maovu. Wanachofanya ni kutuonyesha nani waliyemfundisha ubaya halafu akayakataa masharti yao. Tunashukuru kwa zoezi hilo. Lakini inapofikia mahali pa kuua raia wasio na hatia kufanikisha zoezi la kutuonyesha nani waliyemfundisha ubaya halafu akakosa kuyakubali masharti fulani, hapo ndipo tunapopingana na Amerika. Hatuwezi kuwaruhusu waongeze maovu kupigana na mwovu waliyemtengeneza. Wanajuana wenyewe wamalize matatizo yao bila kuwaangamiza raia wa Iraq wasio na hatia. Tunataka amani, Hatuitaki vita. Wanadamu wenye hekima vita huwa ni hatua ya mwisho kuichukua wakati nyingine zote zimeshindwa. Vita inaharibu mali na maisha ya wanadamu duniani. Itavuruga uchumi wa dunia. Wengi watahusishwa hata kama risasi na bomu hazitawaangukia. Joto la vita litasikika kila mahali. Ndiyo maana katika maombi yetu siku ya leo, Hatuombi kwa ajili ya Raia wa Iraq na wanajeshi wa Amerika ambao watakufa wengi vitani, Bali tunawaombea watu wote duniani. Kwa namna moja au nyingine wameingizwa kwenye vita isiyowahusu. Na mbaya zaidi taifa linalofanya makosa hayo linajiita taifa kubwa kuliko yote duniani. Ikiwa wale waliotegemewa kufanya kwa busara ndio wanaofanya yasiyoeleweka, Je waliotegemewa kufanya kiupunguani watafanyaje? Kabla Bwana Yesu hajarudi, Tutayaona mengi.

Tuombe

Mungu wetu mkuu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Bwana wa majeshi yote ya Mbinguni na Duniani. Tizama watu wako duniani kote. Ni kazi ya mikono yako. Hakuna taifa wala mtu uliyemruhusu kuua watu wako. Ndiyo maana ulisema katika amri zako kwamba mwanadamu asiue. Tunayoyasikia na kuyaona ni matunda ya watu walio na kiu ya kumwaga damu. Hawalali usingizi mzuri kabla hawajamwaga damu za watu wasio na hatia. Waliyayakusudia ndiyo watakayoyafanya hata kama watu wako dunia nzima watapiga kelele za kuwataka waache njia na mbinu zao mbaya. Baba nisamehe kuuliza swali hili kwako. Nani mwenye kuimiliki dunia hii, Amerika? Au wewe muumbaji wetu? Je utawaruhusu watu fulani kwa sababu ya uwezo wao kijeshi na kiuchumi kuua weatakaye kwa wakati watakao? Je wewe ni Mungu wa wenye uwezo pekee? Hapana hatuamini hivyo. Tunaamini kwamba wewe ni Mungu wa kila mwenye mwili duniani bila kujali uwezo wa kiuchumi. Unatupenda sote. Ndio maana tunakuja kwako mtetezi wa wanyonge uwatetee sasa. Kama kuna wakati waliowahi kukuhitaji, Sasa wanakuhitaji kuliko wakati mwingine wowote. Waokoe na makucha ya hao wanaotaka kumwaga damu zisizo na hatia. Wakumbatie kwa mkono wako, na uwatoe kwenye mabaki ya milipuko ya mabomu salama. Hawakutarajia kufa hivyo, usiruhusu wafe hivyo. Unaweza ndio maana tuna ujasiri wa kukuomba.Tunakuamini ndio kwa maana tunayapokea majibu ya maombi yetu. Tuna matumaini ndiyo maana bado kuna wanadamu wanaoishi sehemu inayokabiliwa na vita. Matumaini yote ni kwako. Hawasemi, Pengine hawana ujasiri wa kusema hivyo. Lakini mioyoni mwao hawana tumaini jingine isipokuwa wewe. Wathibitishie matumaini yao kwa kuwaokoa na kuwaifadhi salama. Tunakushukuru kimbele tukijua wewe ni Mungu unaelisimamia neno lako. Ulisema tukuite maadam unasikia. Ndivyo tunavyofanya, na sasa matumaini yetu ni kwako. Yote tumeyaomba kupitia jina la Mwanao Yesu Kristo mwokozi wetu. Amen.

Bonyeza hapa kwa habari zaidi

 
| http://munishi.netfirms.com |